الحجج الدامغة
على استحالة رؤية الله بالأبصار
AL-HUJAJ AL-DAAMIGHA.
HOJA ZENYE NGUVU
JUU YA
KUTOONEKANA MWENYEZI MUNGU
KWA MACHO.
NA:
J.M.R. AL-MAZRUI.
"الله ينجز وعده و يخلف وعيده!!!"
Mwenyezi Mungu anatekeleza ahadi yake njema,
na anakwenda kinyume na
onyo lake!!!"
Sasa tazama Mwenyezi Mungu mwenyewe anavyo sema:
قال لا تختصموا لدي و قد قدمت إليكم بالوعيد *** ما يبدل القول لدي و ما أنا بظلام للعبيد.
(Na) atasema Mwenyezi Mungu musigombane mbele yangu na nilikwisha kukutangulizieni onyo (langu). *** kauli yangu
haibadilishwi kwangu na (wala) Mimi si mwenye
kuwadhulumu waja wangu."
Sura ya 50 aya ya 28-29.
MANENO YA AL-ALUSI, MFASIRI WA QUR'ANI.
Anasema Al-alusi katika tafsiri yake RUH AL-MAANI juzuu ya 9 ukurasa wa 25:
"Amenukuu Al-manawi kwamba Al-kamal bin Al-himam aliulizwa juu ya yale aliyoyapokea Al-darqutni na wengineo kutoka kwa Anas katika kauli yake Mtume (S.A.W.) (inayosema):
"رأيت ربي في أحسن صورة"
"Nimemuona Mola wangu katika sura nzuri yao,"
kwa misingi ya kukufasiri kuona kwa (maana ya) kuona hali ya kuwa macho (yaani si kuona katika usingizi). Akajibu kwamba "hili ni pazia la sura…………na wametaja baadhi yao kwamba Nabii Mussa alikuwa anamuona Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini alikuwa hajui kuwa aliyemuona ndiye Yeye (Mwenyezi Mungu). Na katika njia hii zinafasirika baadhi ya riwaya zilizopondwa (yaani zilizokataliwa na baadhi yao, zenye kusema kuwa)
"رأيت الله في صورة الشباب __و في بعضها زيادة__ له نعلان من ذهب "
"Nimemuona Mola wangu katika sura ya kijana--na katika riwaya nyengine kuna ziada (inayosema kwamba --- naye (Mwenyezi Mungu) ana viatu viwili vya dhahabu!!!"
Basi yatakaposihi (yatakapokuwa sahihi) yaliyosemwa na Mashekhe na yalivyofahamisha maneno ya Al-suyuti, mimi, namshukuru Mwenyezi Mungu, nimemuona Mola wangu usingizini mara tatu. Na ilikuwa mara ya tatu mwaka wa 1246 A.H. Nimemuona Mola Mtukufu naye ana nuru anaelekea upande wa mashariki, akanisemesha maneno nimeyasahau nilipoamka!!!"
1) Mwenyezi Mungu ana sura nzuri yao!!!
2) Mwenyezi Mungu ana sura ya kijana!!!
3) Mwenyezi Mungu ana viatu vya dhahabu!!!
4) Yeye kamuona Mwenyezi Mungu usingizini mara tatu. Mara ya tatu anaelekea mashariki, na akamsemesha!!!
5) Nabii Mussa alikuwa anamuona Mwenyezi Mungu!!!
Hapa Al-alusi kasahau maneno ya Mwenyezi Mungu alipomwambia Nabii Mussa katika Qur'ani Sura ya 7 aya ya 143 kuwa:
"لن تراني"
"Hutoniona."
Yeye ananukuu maneno ya mashekhe wenye kusema: "sio hivyo, bali alikuona!!!"
MANENO YA IBN BATTA.
Anasema Ibn Batta kwamba: "Nabii Mussa alimkuta mtu juu ya mti kavaa vazi la sufi na viatu akasema naye, yaani yule mtu akasema na Nabii Mussa. Nabii Mussa akasema ni Muibrania gani huyu anayesema na mimi, yule mtu akajibu "mimi ni Mwenyezi Mungu." Yaani Nabii Mussa kamkuta Mwenyezi Mungu katia suti na viatu. Hii si kufuru ni nii? Tazama "LISAN AL-MIZAN" cha Ibn Hajar juzuu ya 4 ukurasa wa 131.
Ibn hajar naye pamoja na elimu yote aliyokuwa nayo na ubingwa mkubwa wa hadithi, lakini kasema maneno yamewastaajabisha wanavyuoni wengine. Na kilichomfanya aseme maneno haya si jengine bali ni itikadi yake ya kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana. Anasema katika kitabu chake FATH AL-BARI juzuu 13 ukurasa wa 433:
"Na maana ya hadithi ya mlango (huu) ni kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu na kutosheka kwake, (basi) asimuone yeyote (katika viumbe Wake). Lakini rehema yake inamaanisha kuwa awaoneshe Dhati Yake kwa kuikamilisha neema. Basi kitapoondoka kizuizi (pazia baina ya Mwenyezi Mungu na viumbe) atawafanyia (kitu) kinyume na utukufu wake!!!
Labda tuweke wazi kidogo. Anasema Ibn Hajar kuwa maana ya hadithi hii (yaani hadithi inayosema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani) ni kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu unamaanisha kuwa asionekane na kiumbe yeyote, lakini rehema yake itamfanya aende kinyume na utukufu wake na kwahivyo ajidhihirishe kwa viumbe wake!!! Sasa wewe zingatia maneno haya AENDE KINYUME NA UTUKUFU WAKE. Haya ni maneno ya Ibn Hajar, nayo yana hatari ndani yake. Vipi Mwenyezi Mungu afanye kitu kinyume na utukufu wake. Haya yote kayasema katika kuilazimisha itikadi ya kuonekana kwa Mwenyezi Mungu.
MANENO YA SAYYID MUHAMMAD RASHID RIDHA, MFASIRI WA QUR'ANI: NAKALA KUTOKA KWA SH. AL-KHALILI.
"Basi jua kwamba umeme na vile alivyovijaaliya Mwenyezi Mungu kuwa ni chanzo cha kuumba ulimwengu ndio pazia linalozuia Mwenyezi Mungu asionekane!!!" Na kwamba kufunuliwa kwa pazia hili hakutokuwa ila katika pepo."
Tazama dunia hii! Al-alusi ananukuu maneno ya mashekhe wakisema kuwa Nabii Mussa kamuona Mwenyezi Mungu, wakati Mwenyezi Mungu katika Qur'ani anakataa kwa kumwambia Nabii Mussa kuwa "hutoniona," na Sayyid Muhamed hapa anasema kuwa: "umeme na yale ambayo Mwenyezi Mungu kayajaalia kuwa ndio chimbuko la maumbile ndio vilivyofanya kuwa Mwenyezi Mungu asionekane” wakati Mtume (S.A.W.) anasema katika hadithi sahihi kwamba: "utukufu wa Mwenyezi Mungu ndio uliozuia Mwenyezi Mungu asionekane." Kwa maneno mengine ni kuwa kwa mujibu wa maneno ya Sayyid Muhamed Mwenyezi Mungu kajiziba na sisi kwa kutumia baadhi ya viumbe vyake!!! Na yote haya kayasema kwa sababu ya itikadi yake ya kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana.
MANENO YA DR. ABDRAHIM AL-TAHAN.
Dr. Al-tahan aliitisha muhadhara wake U.A.E, akidai kuwa anawajibu wale wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani. Japo kuwa wakiitwa yeye na wenzake kwenye mjadala wa wazi hukimbia, lakini wakiwa peke yao wanakuwa wasemaji wakubwa. Na katika muhadhara huo aliporomoka sana: alikuwa akitoa hadithi maudhui (ya kutunga) akisema kuwa ni hadithi hasan "chini ya hadithi sahihi kidaraja, lakini zote zinakubalika." Na alikuwa akitoa hadithi dhaifu tupu kama utakavyoona humu Mwenyezi Mungu akipenda. Bali hakujibu hata hoja moja ya wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani. Na hatima yake akasema maneno ambayo mbingu na ardhi zinakaribia kupasuka kwa maneno hayo. Anasema Dr. Al-tahan:
"Hakuna kheri katika Qur'ani isipokuwa kwa suna (hadithi) na hakuna kheri katika suna isipokuwa kwa kuwafahamu wanavyuoni wetu waliotangulia. Na kila anayelingania katika Qur'ani bila ya suna basi ni mpotovu na kila anayelingania katika Qur'ani na suna bila ya kuwafahamu wanavyuoni wetu waliotangulia basi ni mpotovu!!!"
Haya ndio maneno ya DR. Al-tahan. Kwahivyo, kwa mujibu wa Al-tahan, Qur'an - hadithi = haina kheri; Qur'an + hadithi - maneno ya watu = hazina kheri!!! Haya yote kayasema kwa sababu lazima Mwenyezi Mungu aonekane, na yeye ndio yumo katika kuwajibu wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani. Masikini Al-tahan!
Labda mtu anaweza akasema kwamba makusudio ya Al-tahan ni kwamba kuna watu hawataki hadithi za Mtume: wanachukua Qurani tu, haya ndio makusudio yake. Lakini jawabu ni kuwa:
1) Yeye Al-tahan katika muhadhara wake huo aliyoporomoka na kuonesha uchache wa elimu yake anadai kwamba anawajibu Maibadhi (AHLU AL-HAQI WAL-ISTIQAMA). Sasa wapi kaona au lini kasikia kwamba Ibadhi wanakataa hadithi za Mtume (S.A.W.)?
2) Al-tahan hakusema kuwa mtu anayeacha hadithi na kutoa hoja kwa Qur'ani tu kuwa ndio mpotovu, bali kasema kuwa katika Qur'ani na hadithi hakuna kheri mpaka uwafahamu wanavyuoni wao waliotangulia. Kwahivyo kutegemea Qur'ani na hadithi tu haifai ni lazima upate na maneno ya mtu!!!
Haya ni maneno walioyasema kuhusu kuitetea itikadi ya kumuona Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu akipenda utaona baadae maneno ya Ibn Al-qayyim kuhusu itikadi ya kutoka motoni. Sasa baada ya haya nitakupa mifano mwyengine ya itikadi mbovu sana ambazo tayari wanazo baadhi ya ya waislamu ukitoa itikadi mbili hizi nilizokutajia: za kumuona Mwenyezi Mungu na kutoka motoni. Na itikadi hizi ambazo nitakutajia sasa hivi (Inshala) zimo hasa katika madhehebu ya kiwahabi na wao wamezirithi kutoka kwa Maimamu wa madhehebu za Al-hashwiya Al-mujasima kama Ibn Taymiyya, Ibn Qayyim Al-jawziya na wengineo. Natuanze kwa kuitazama falsafa ya Ibn Teimiya kuhusu maumbile ya ulimwengu.
FALSAFA NA ITIKADI YA IBN TAYMIYYA.
Na akitegemea hadithi za uwongo, Ibn Taymiyya katika kitabu chake AL-AQIDA AL-WASTIYA ukurasa wa 12, anasema kwamba:
1) Jahanam haiachi kutupwa (waovu) ndani yake nayo inasema ongeza mpaka Mwenyezi Mungu atatia mguu wake nadani yake!!!"
2) Kisha anasema Ibn Taymiyya kuwa (Mwenyezi Mungu) "anaendelea kucheka."
Na akasema Ibn Al-qayyim katika kitabu chake hicho ukurasa wa 299: " Mwenyezi Mungu anacheka na kufurahi!!! Na nyoyo ya waja iko katika vidole viwili miongoni mwa vidole vyake!!! Na kamuumba Adam kwa sura yake!!! (yaani Mwenyezi Mungu ana sura kwa sura hio ndio kaitumia kuchukuwa kigezo cha kuumba sura ya Adam)!!! Anaendelea kwa kusema: "na mbingu na ardhi siku ya kiama zitakuwa kiganjani chake!!! "Na ataweka MGUU wake kwenye moto….na atawatoa watu kwenye moto kwa mkono wake!!!"
Ibn Al-qayyim na Mashekhe wake na wafuasi wake wanayasema haya kwa uhakika wake, sio kwa kuyaletea tafsiri bali tukisema kwamba Mwenyezi Mungu ana mkono ni kuwa kweli anao mkono lakini hatujui umekaaje wala haufanani na kitu!!! Sasa tunamuuliza huyu aliyesema maneno haya je yeye ni mfuasi wa nani? Kwa sababu yeye anasema kuwa wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani basi ni wafuasi wa Fir’awna, kama tutakavyo nukuu maneno yake baadae Mwenyezi Mungu akipenda. Sasa tazama huyu ndio Imamu wa Mawahabi ana itikadi kama hizi, wafuasi watakuwa na itikadi gani? Huyu ni mmoja katika Maimamu wakubwa wa kiwahabi. Sasa na tumtazame Imamu wa pili katika Maimamu wao naye ni Uthman Al-darimi.
MANENO YA UTHMAN AL-DARIMI.
Uthman Al-darimi alimjibu Bishri Al-marisi mwanachuoni wa kihanafi maneno makali kwa sababu ya itikadi yake ya kumtakasa Mwenyezi Mungu kutokana na sifa za viumbe. Kwa hakika yeye Uthman Al-darimi ndiye anayehitaji kujibiwa sio yeye ajibu, kwani ukisoma hio jawabu yake utaona kizungu zungu. Soma baadhi ya nakala zake kutoka katika kitabu chake hicho. Anasema Uthman Al-darimi:
1) "Mwenyezi Mungu) kamuumba Adam kwa kumshika!!! Tazama kitabu “RADU AL-IMAMU AL-DARIMI ALAA BISHRI ALMARISI.” Ukurasa wa 25.
3) "Hakika yake (Mwenyezi Mungu) anakaa kitako juu ya kiti basi haibakii (nafasi) isipokuwa kiasi cha vidole vinne."!!!! Ukurasa wa 74.
4) "Mwenyezi Mungu….anaondoka (anafanya harakati) akitaka, na anapanda juu na kushuka chini akitaka."!!! Ukurasa wa 20.
5) “Na imetufikia kwamba wao (malaika wenye kuibeba Arshi ya Mwenyezi Mungu) walipoibeba (hio Arshi) na juu yake alikuwako (Mwenyezi Mungu) Jabari katika utukufu wake!!! Kwahivyo hapa kiti kimebebwa na Malaika na Mwenyezi Mungu yuko juu kabebwa mzega mzega!!!! Tazama ukurasa wa 85.
6) “Lau (Mwenyezi Mungu) alitaka basi angebebwa na bawa la mbu…….basi vipi wewe mwenye kibri (yaani Bishri Al-marisi) unakanusha kwamba Arshi haiwezi kumbeba?!!!” Ukurasa 85.
7) Mwenyezi Mungu ana vidole. Tazama maneno yake kwa urefu kuanzia ukurasa wa 59.
8) “Kiti ndio sehemu ya (kuwekea) miguu yake miwili (yaani miguu ya Mwenyezi Mungu)!!! Ukurasa wa 67.
Sasa tazama alivyosema Uthman Al-darimi huyu alipomjibu Bishri Al-marisi. Al-marisi alisema kwamba “Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia wala hana sikio, na ni mwenye kuona wala hana jicho.” Bishr Al-marisi kusema hivi ilikuwa ni dhambi kubwa na yalimchongea sana. Uthman Al-darimi akamjibu Bishr kwamba: “anaambiwa Al-marisi huyu mpotovu (kwamba) punda na mbwa ni bora kuliko Mwenyezi Mungu mwenye sifa hii!!!!” Astaghfiru Al-ah wa Atubu Ilayh. Tazama ukurasa wa 41 katika mlango wa sifa ya kusikia na kuona.
Baada ya haya yote utaona kwamba Uthman Al-darimi, miongoni mwa maimamu watangulizi wa kiwahabi, yeye ndiye anayehitaji kujibiwa sio ajibu. Hizi ndio itikadi zake kiufupi lakini mtu na asome kitabu chake hicho ataona ajabu nyingi.
NAKALA KUTOKA KATIKA KITABU AL-SUNNA
AMBACHO KIMENASIBISHWA KWA
IBN AHMAD.
Kitabu hicho kinasema:
1) "Na kukaa kwa (Mwenyezi Mungu) si vyengine bali ni kukaa kitako."!!! Ukurasa wa 5.
2) "Mola akikaa kitako juu ya kiti, basi husikilikana sauti yake kama sauti ya soji (matandiko ya farasi) ya chuma." Ukurasa wa 70.
3) "Mwenyezi Mungu ameiandika Taurati kwa mkono wake na huku ameegemeza mgongo wake kwenye jabali, sauti ya kalamu inasikika, hakuna baina yake (Mwenyezi Mungu) na baina yake (Nabii Mussa) isipokuwa pazia."!! Ukurasa wa 67.
4) "Hakika ya Mwenyezi Mungu hakumshika kwa mkono wake isipokuwa Adam, kamuumba kwa mkono wake, na pepo, na taurati kaiandika kwa mkono wake na Mwenyezi Mungu amechanganya lulu kwa mkono wake!! Ukurasa wa 68.
5) "Kamuona (Mwenyezi Mungu) juu ya kiti kimebebwa na Malaika wanne. Malaika mmoja sura ya mtu, na mmoja sura ya simba, na mmoja sura ya ng'ombe dume na mmoja sura ya ndege anaitwa "NASR" (aina ya ndege)." Ukurasa wa 35.
6) "Na mkono wake (mkono wa Mwenyezi Mungu) wa pili mtupu hauna kitu."!!! Ukurasa wa 164.
7) "Akaipa wahyi milima kwamba mimi nitateremka katika mlima mmoja katika nyinyi. Basi milima ikafanya kibri, na Mlima Sinai ukanyenyekea na kusema: 'ikiwa kuna kitu nimeandikiwa basi kitanijia.' Basi Mwenyezi Mungu akaupa wahyi kuwa Mimi nitateremka juu yako kwa sababu ya unyenyekevu wako na kuridhika kwako na makadirio yangu."!!!ukurasa wa 149.
9) "Mwenyezi Mungu atashuka katika kivuli cha mawingu kutoka katika Arshi, atajimithilisha (atajigeuza) atawajia………na Mola yuko mbele yao mpaka wavuuke."!!! Ukurasa wa 77. Yaani haya yatatukia siku ya kiyama. Mwenyezi Mungu:
a) atabebwa na mawingu. Aliyesema hivi hakuufahamu muradi wa aya.
b) Atajigeuza. Lakini kumbuka kwamba kubadilika ni sifa ya viumbe: Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu katika dhati yake na sifa zake hazidi wala hapunguwi Yeye ni mkamilifu hana haja ya ziada: kuzidi ni alama ya kasoro.
c) Atakuwa mbele na watu wako nyuma yake mpaka awavuushe kwenye daraja ya jahanam!!!!
9) "Basi akawa Mola wako anazunguka katika ardhi."!!! Ukurasa wa 156.
10) "Hakika ya jahanam ina daraja saba, Mwenyezi Mungu yuko katika (daraja) ya nne katika hizo, watapita viumbe juu ya Mwenyezi Mungu naye yupo katika daraja ya nne."!!!ukurasa wa 182. Linganisha na maneno ya mwanzo kwamba Mwenyezi Mungu atakuwa mbele na watu wako nyuma!!! Tazama hapa tayari sasa wanapita juu yake: yeye yuko chini watu wanapita juu – mgongano wa wazi!!!
11) Kisha (Mwenyezi Mungu) atakuja baada ya hapo hali anakwenda kwa miguu."!!! Ukurasa wa 47.
Tunawauliza wale ambao wana itikadi hizi ambao wanawaita wale wasio amini kuonekana kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni wafuasi wa Fir’awna, je wao ni wafuasi wa nani? Na wanakwenda wapi? Na nini tofauti baina ya itikadi hizi na itikadi za kiyahudi na kinasara? Na mimi ninavyojua Fir’awna alikuwa akiamini kuonekana kwa Mwenyezi Mungu na kwahivyo akamwambia waziri wake Haman “hebu nijengee mnara nimchungulie Mwenyezi Mungu wa Musa.” Basi Ibn Al-qayyim alotwita sisi kuwa ni “wafuasi wa Fir’awna” ni bora yeye jina hili la “mfuasi wa Fir’awna” linamfaa zaidi, kwani Fir’awna haja kataa kuonekana kwa Mwenyezi Mungu.
MANENO YA SH. BIN BAZ.
Anamesema Sh. Abdul-aziz bin Baz katika maelezo yake juu ya KITAB AL-TAWHID: "na katika haya kuna kuthibitisha sifa na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu ana mkono wa kulia na wa kushoto, na kwamba mikono yote ni kulia kama ilivyokuja katika hadithi. Na umeitwa mmoja wa kulia na mwengine wa kushoto kama ni jina tu, lakini kimaana na kisheria yote ni ya kulia na wala hakuna upungufu wa kitu katika hio (mikono miwili)."!!!
Tazama anavyo jigonga: mikono miwili wakulia na wakushoto lakini mkono wa kulia!!! Ni sawa sawa na kusema mikono miwili lakini mkono mmoja!!! Haya ndio kama yale aliyo yasema Sh. Ahmad Deedat kuhusu manasara wanaposema kwamba: “Baba ni Mwenyezi Mungu, Mwana ni Mwenyezi Mungu na Roho mtakatifu ni Mwenyezi Mungu lakini hakuna miungu mitatu bali kuna Mwenyezi Mungu mmoja!!!”
MANENO YA SH. AL-UTHAIMIN.
"Na kwa hali yoyote ile, hakika ya mikono yake Mwenyezi Mungu ni miwili hapana shaka. Na kila mmoja sio mwengine. Tukiuita mkono wake mwengine kuwa ni wa kushoto, muradi sio kuwa una nguvu kidogo kuliko wa kulia, bali mikono yake yote miwili ni kulia."!!! SHERH KITAB AL-TAWHID juzuu ya 3 ukurasa wa 297.
Na aliulizwa Sheikh huyu "je kweli Mwenyezi Mungu anachoka?" Akasema "ndio" lakini kuchoka kwake si kama kuchoka kwetu!!! Sasa soma suala na jibu hilo kutoka katika kitabu chake cha fatawa "Fatawa Al-aqida" ukurasa wa 51-52.
س: هل نفهم من حديث "إن الله لا يمل حتى تملوا" –متفق عليه- أن الله يوصف بالملل؟"
Suala: "Je tunafahamu kutoka katika hadithi (inayosema kwamba) "hakika ya Mwenyezi Mungu hachoki mpaka muchoke" kwamba Mwenyezi Mungu anajisifia kwamba (Yeye) anachoka?" الجواب: "من المعلوم أن القاعدة عند أهل السنة و الجماعة أننا نصف الله تبارك و تعالى بما وصف به نفسه من غير تمثيل و لا تكييف . فإذا كان هذا الحديث يدل على أن لله مللا فإن ملل الله ليس كمثل مللنا نحن بل هو ليس فيه شيء من النقص." Jawabu: "Inajulikana kwamba kawaida ya Ahlu-suna wal-jamaa kuwa sisi tunamsifu Mwenyezi Mungu kwa (sifa) aliyojisifu Mwenyewe bila ya kummithilisha wala kumfananisha. Ikiwa hadithi hii inaonesha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anachoka basi (jua) kwamba kuchoka kwake si kama kuchoka kwetu sisi; bali huko (kuchoka kwake ni kuchoka ambako) ndani yake hakuna upungufu wa namna yoyote!!!"
Hizi ndio baadhi tu ya itikadi za Mawahabi, Mwenyezi Mungu awaongoze. Kwahivyo tunapata katika itikadi hizi za Mawahabi kwamba Mwenyezi Mungu ana uso, mikono, miguu, macho, mgongo, anacheka, anakwenda katika ardhi, anakaa kitako, anabebwa na Malaika Naye yuko juu ya kiti na atakaa katika daraja ya nne ya jahanam hali ya kuwa watu wanapita juu yake!!!
Sasa unaweza ukajiuliza kwanini watu hawa wakawa na itikadi hizi: nini chanzo chake? Jawabu ya suala hili utaipata katika sehemu inayofata.
CHANZO CHA KUTUMBUKIA KATIKA
ITIKADI HII BATILI.
Sababu kubwa na chanzo cha Mawahabi kuwa na itikadi hizi za kumfananisha Mwenyezi Mungu na viumbe, wakasema kuwa Mwenyezi Mungu ana mikono, miguu, uso, macho, anakwenda kwenye ardhi, anacheka, anakaa kitako kweli kweli, aliegemeza mgongo wake kwenye jabali huku akiandika Taurati, n.k., ni kukanusha kwao kuwepo kwa majazi katika lugha ya kiarabu na hasa hasa katika Qur,ani. Miongoni mwa walioandika kwa urefu na kukataa jambo hili ni Ibn Qayyim Al-jawziyya katika kitabu chake “MUKHTASAR AL-SAWAAIQ AL-MURSALA” juzuu ya 2 inaanzia ukurasa wa 231. Na unwani “heading” ya sehemu hio ni “SEHEMU YA KUMVUNJA TAGHUTI (SHETANI) WA TATU…NAYE NI TAGHUTI WA MAJAZI.” Na maana ya "majazi" ni kutumika neno tafauti na maana yake ya asili. Kwa mfano neno "simba." Neno hili linamaanisha aina maalumu ya mnyama wa porini. Na hii ndio maana yake ya asili. Lakini nikisema Ali ndio simba wa kijiji hiki, makusudio huwa siyo yule mnyama wa porini, bali ni kuwa Ali ni shujaa wa kijiji hiki. Na hii ndio maana ya "majazi": kutumika neno kinyume na maana yake ya asili. Sasa wao Mawahabi wanakataa kuwa katika Qur'ani hakuna majazi. Kwahivyo Mwenyezi Mungu aliposema:
"يد الله فوق أيديهم"
"Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao,"
Sura ya 48 aya ya 10.
wao wakasema kuwa Mwenyezi Mungu ana mkono. Masikini hawa hawakuifahamu Qur'ani wala lugha ya kiarabu iliotumika kuteremshiwa Qur'ani. Sasa kwanini basi wakasema kuwa Mwenyezi Mungu ana mikono miwili tu na aya ziko ziliozoonesha kuwa mikono yake ni mingi zaidi ya miwili? Anasema Mwenyezi Mungu:
"والسماء بنيناها بأيدٍ"
"Na mbingu tumezijenga kwa mikono yetu (mingi zaidi ya miwili)."
Sura ya 51 aya ya 47.
Sasa tafsiri na iwe hivi "Mwenyezi Mungu ana mikono mingi zaidi ya miwili" kama aya hii inavyosema. Na alipotaja mkono mmoja basi iwe kataja mmoja katika hio mingi na halkadhalika alipotaja miwili awe kataja miwili katika hio mingi, lakini kwa mujibu wa aya hii mikono yake ni mingi zaidi ya miwili." Sasa kama ni hivi kwanini tena waseme ana mikono miwili tu? Ukiniambia kwamba “lugha ya kiarabu inatumika katika wingi (tatu na kuendelea) kumaanisha mbili, na mbili kumaanisha wingi (tatu na kuendelea) na moja kumanisha wingi vile vile.” Nitakujibu kwamba:
1) Katika lugha ya kiarabu pia unatumika mkono kumaanisha nguvu, neema, uwezo n.k., kama utavyoona humu.
2) Kama unakubali kwamba wakati mwengine moja hutumika kumaanisha nyingi, basi umejijibu mwenyewe kwani haya ndio majazi yenyewe unayoyakataa: kutumika neno kinyume na maana yake ya asili. Kwani kwa asili moja ni moja ikitumika kumaanisha tatu basi imetumika kinyume na maana yake ya asili.
Lakini haya yote yanatujuilisha kwamba hawa watu Mwenyezi Mungu hakuwapa nuru hata kidogo ya kukifahamu Kitabu chake. Sasa ukitaka kujua kwamba neno mkono katika lugha ya Qur'ani hutumika si kwa maana ya mkono wa kweli, soma aya hizi zinazofata kisha tia akilini, utafakari, uzingatie na kujiuliza je mkono uliotajwa katika aya hizi ni mkono wa kweli. Anasema Mwenyezi Mungu:
"ولا تجعل يدك مغلولة إلى عنقك ولا تبسطها كل البسط"
"Wala usiufanye mkono wako kuwa wenye kufungwa kwenye shingo yako wala usiukunjue wote." Sura ya 17 aya ya 29.
Je neno "mkono" hapa ni mkono wa kweli au maana yake ni kuwa usifanye ubakhili wala usifanye israfu? Kama ni mkono kweli kweli ndio uliokusudiwa hapa, basi mbona wenye kukataa majazi hawatembei na huku mikono yao ipo kati na kati tu baina ya shingo na kuukunjua wote?
Na anasema Mwenyezi Mungu:
"و اذكر عبدنا داود ذا الأيد"
"Na mkumbuke mja wetu Daudi mwenye mikono
(yaani mwenye nguvu). Sura ya 38 aya ya 18.
Sasa je neno "mikono" hapa maana yake ni mikono hii ya viungo? Kama ndio basi Nabii Daud alikuwa na mikono zaidi ya miwili kwa sababu aya inasema ""ذا الأيد (mwenye mikono mingi zaidi ya miwili). Bali hapa mikono maana yake ni nguvu.
Na akasema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani:
و اذكر عبادنا إبراهيم و إسحاق و يعقوب أولي الأيد و الأبصار" "
"Na wakumbuke waja wetu Ibrahim, na Is'haq na Ya’aqub wenye mikono na macho." Sura ya 38 aya ya 45.
Katika aya hii Mwenyezi Mungu anamtaka Mtume Wake awazingatie Mitume hawa kwa sababu Mwenyezi Mungu kawapa mikono na macho. Sasa kwani sisi hatuna mikono na macho? Kwahivyo mikono hapa maana yake ni nguvu na macho ni busara na uwezo mkubwa wa kutazama mambo, kuyatafakari na kuyafahamu mambo hayo pamoja na hekima. Sasa kama Mawahabi wanakataa kuwepo kwa majazi ninawaomba wazingatie aya hizi na nyengine nyingi ambazo maneno yametumika kinyume na maana yake ya asili. Wala hili si jambo la kushindana na kufanya ari: sisi ni Waislamu, watoto wa familia moja tuko katika kufahamishana ukweli.
Kwahivyo mkono wa Mwenyezi Mungu maana yake ni nguvu za Mwenyezi Mungu sio kiungo kama wanavyosema wao. Na hivi ndivyo lugha ya kiarabu inavyosema. Anasema babu yake Mtume (S.A.W.) wakati Mtume (S.A.W.) alipopotea katika mji wa Makka alipokuwa mdogo. Babu yake Mtume aliimba mashairi haya:
"رد علي ولدي محمداً***اردده ربي و اجعله لي يداً"
"Nirejeshee (é Mwenyezi Mungu) Muhammad mwanangu ***mrejeshe é Mola wangu na umfanye kuwa mkono wangu."
Sasa vipi Mtume (S.A.W.) afanywe kuwa mkono wa babu yake. Hapa babu yake Mtume anamuomba Mwenyezi Mungu amfanye Muhammad (S.A.W.) kuwa ni sababu ya yeye kupata nguvu au awe ni neema kwake.
Na kwakufahamu zaidi kuwepo kwa majazi katika Qurani soma aya hii:
"وكلوا و اشربوا حتى يتبين لكم الخيط الأبيض من الخيط الأسود"
Aya hii inahusu mwezi wa Ramadhani, anasema Mwenyezi Mungu katika aya hii:
"Na kuleni na kunyweni mpaka ukubainikieni uzi mweupe kutokana na uzi mweusi." Sura ya 2 aya ya 187.
Sasa tunawauliza wanaokataa majazi je nyuzi hizi mbili nyeupe na nyeusi zilizotajwa katika aya hii ni nyuzi kweli? Jawabu ni kuwa hizi sio nyuzi kweli kama za kushonea nguo, bali uzi mweupe ni kuchomoza kwa alfajiri sahihi ambayo huanza weupe katika upeo wa macho na uzi mweusi ni kiza cha usiku- na kwa maana hio maneno "nyuzi" katika aya hii si hakika bali ni majazi (mithali). Hii ni aya ambayo mmoja ya sahibu zangu alimtolea mtu mmoja anayekanusha majazi, na ikawa hana jawabu.
Na Al-imamu Nur Al-din Al-salimi anasema katika kitabu chake “Talat Shams” juzuu ya 1 ukurasa wa 206 alipokuwa akizungumzia habari ya majazi kwamba Abu Tamam katika washairi wa zamani alitoa ushairi wake akasema: "لا تسقني ماء الكأبة" (usininyweshe maji ya huzuni). Ikawa kuna mtu pale katika wanaopinga majazi. Akasema yule mtu kumwambia Abu Tamam “haya nipe hio glasi yako nikutilie maji ya huzuni.” Yaani anakusudia kumwambia “tangu lini wewe umesikia kwamba huzuni inanywewa?” Abu Tamam akamjibu yule mtu akamwambia “haya huu mkasi nikatie bawa lako la udhalili.” Abu tamimi naye anaikusudia kumjengea hoja kwa kutumia aya inayosema kwamba “na wainamishie (wazazi wako wawili) bawa la udhalili.” Yaani je bawa hapa ni bawa la kweli, na tangu lini na wapi umesikia kwamba mtu ana bawa? Kama si bawa basi elewa kwamba haya yote ni katika majazi ya lugha ya kiarabu.
Na mimi siku moja nilijadiliana na hao wenye kukataa majazi. Nikamwambia yule bwana kama wewe unakataa majazi hebu soma aya hii:
""واعتصموا بحبل الله حميعا
"Na kamataneni na kamba ya Mwenyezi Mungu kwa pamoja."
Sura ya 3 aya ya 103.
Nikamwambia haya niliyetee hio kamba ya kweli kweli ya Mwenyezi Mungu tukamatane nayo. Ikawa hana jawabu isipokuwa kuniambia kuwa "maudhui hii inataka utafiti." Sasa tazama je kamba hapa katika aya hii ni kamba ya kweli? Kila mtu anajua kuwa kamba hapa ni dini sio kamba ya kufungia ng'ombe. Sasa ikiwa umeyafahamu haya basi elewa kuwa makusudio ya mkono wa Mwenyezi Mungu ni nguvu Zake. Uso ni Dhati Yake, au katika sehemu nyengine limetumika neno "uso" kwa maana ya radhi zake. Macho kwa maana ya hifadhi yake. Na hivyo hivyo kila kitu kinafasiriwa tafsiri inayokubaliana na sifa za Mwenyezi Mungu.
ZINGATIA.
Sasa baada ya kusoma maneno hayo ya Maimamu wa kiwahabi, nadhani utakuwa umeelewa hatari iliowakabili Waislamu. Watu wengi walioko Afrika ya Mashariki na Kati hawajui kama hizi ndio itikadi za Kiwahabi. Fikra zao zote ni kuwa tofauti baina ya Mawahabi (wanaojiita kila jina mara Ansar suna, mara salafia, mara Ahlu suna) ni kufunga tu: kwamba watu wa madhehebu nyengine wanasema tusifunge mpaka mwezi uonekane katika nchi yetu, na Mawahabi wanasema "tufunge ukionekana popote." Basi kila mwenye kuiwafiki rai hii utaona haraka anakimbilia katika kambi ya kiwahabi. Sasa changu mimi ni kukuzindueni kuwa hizi ndio itikadi za kiwahabi na hizo nakala kutoka kwa Maimamu wao akiwemo Bin Baz Mufti aliyepita wa Saudia. Nimezinukuu kiufupi na kwa urefu zaidi utazipata katika barua yangu ya wazi niliyompelekea mmoja ya mashekhe wetu wa Zanzibar. Kwahivyo tahadharini, kuna hatari ya mtu kupoteza Uislamu bila ya kujua.
MAUDHUI YA KITABU HIKI.
Maudhui ya kitabu hiki ni moja katika Mas'ala muhimu katika itikadi ya kiislamu. Maudhui hii ni mas'ala ya kuonekana au kutoonekana kwa Mwenyezi Mungu. Waislamu wametofautiana sana juu ya jambo hili. Kuna wengine wanaamini kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana na wengine wanaamini kuwa haonekani. Na mashuhuri katika wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani duniani wala akhera ni Maibadhi "Ahlu Al-haqi Walistiqama." Na sifa kubwa ya madhehebu hii katika mas'ala ya itikadi, ni kumtakasa Mwenyezi Mungu na sifa zote za viumbe. Na wao hawana tofauti hata moja katika mambo ya itikadi kutokea Maimamu wao wa mwanzo, Jabir bin Zaid, Abu Ubaida, Al-rabii bin Habib, Suhar Al-abdi na wegi wengineo katika Maimamu wao wa mwanzo, mpaka kufikia leo hii, katika zama za Al-khalili na Al-qannubi.
Lakini wenzao wa madhehebu neyngine zote, basi huwepo tofauti baina yao katika masala ya itikadi. Na kwahivyo wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana nao pia wanatafautiana. Wengi wao wanasema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani duniani lakini ataonekana akhera. Na wengine wanasema inawezekana kwa Mwenyezi Mungu akaonekana hata duniani. Na hawa pia wanatafautiana: je kumuona Mwenyezi Mungu hapa duniani ni kwa ajili ya Mtume (S.A.W.) tu au na Waumini pia wanaweza wakamuona? Wengi wanasema kuwa kumuona Mwenyezi Mungu duniani ni kwa ajili ya Mtume (S.A.W.) tu. Na hawa wameisahau hadithi ya Bibi Aaisha na Mtume (S.A.W.) mwenyewe alipoulizwa: “je umemuona Mola wako” akasema kuwa: “sikumuona.” Bali wamesahau aya ya Qur'ani Mwenyezi Mungu aliposema kuwa "haiwi kuwa binaadamu azungumze na Mwenyezi Mungu ila iwe nyuma ya pazia au atume mjumbe (Malaika) ampe wahyi." Sura ya 46 aya ya 51. Na wengine wanasema hata waumini inawezekana wakamuona. Na hawa nao wameyasahau yaliyomfika Nabii Mussa alipoomba kumuona Mwenyezi Mungu. Na sijui kuna muumini gani aliyewashinda Mitume. Na waliosema kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana akhera wakakhitalifiana tena: je ataonekana na Waumini tu au na wanafiki pia? Wengine wakasema ataonekana na Waumini tu. Na kauli hii inagongana na hadithi zao nyingi walizozitegemea ambazo zinasema kuwa wanafiki pia watamuona Mwenyezi Mungu, kama tutakavyo zinukuu Mwenyezi Mungu akipenda. Na wengine wakasema watamuona waumini na wanafiki kama zinavyosema riwaya nyingi. Lakini na hili pia linagongana na itikadi yao pamoja na riwaya zao nyengine nyingi zinazosema kuwa kumuona Mwenyezi Mungu ndio neema kubwa kuliko zote katika neema za akhera. Sasa kama wanafiki wameshapata neema kuu yao nayo ni kumuona Mwenyezi Mungu kipi kitakacho wafanya wasipate neema ndogo ya pepo? Na wakakhitalifiana tena: je wanawake watamuona Mwenyezi Mungu au hawamuoni? Wengine wanasema kuwa hawamuoni, na wengine wanasema na wao pia watamuona.
Na ikiwa mtu anatumia akili yake basi mgongano huu baina ya watu wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana peke yake unatosha kuonesha kuwa hawakukamatana na msingi madhubuti. Na kwa sababu hii unakuta wengine wanapenda kuwatukana wale wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani, lakini hawawezi kujadiliana nao. Mfano mzuri wa hili ni mkutano wa Sheikh Al-mufasirin Al-alama Al-rabani Ahmad Al-khalili, Mufti wa Oman, na Sh. Bin Baz, Mufti wa Saudia. Na kabla sijakunakilia mazungumzo yao kwanza nitakunakilia maneno ya mmoja katika Maimamu wakubwa wa Sh. Bin Baz uone anavyowatukana watu wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani.
MANENO YA IBN AL-QAYYIM
Anasema Ibn Al-qayyim kuhusu watu ambao wanasema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani kuwa wao ni "watu wa bidaa, na wenye kutoka katika dini, na Jahmiya, na ni wafuasi wa Fir’awna wenye kuzikataa sifa za Mwenyezi Mungu, na wametoka katika dini zote, na wamekamatana na kamba ya shetani, na wamekatikiwa na kamba ya Mwenyezi Mungu, na wanazipiga vita suna na watu wenye kuzifuata, na wanampa amani kila adui ya Mwenyezi Mungu na (adui wa) Mtume wake na (adui wa) dini yake, na wote hawa (ambao hawaamini kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana) basi watazuiliwa kutokana na Mola wao, hao ndio wafuasi wa upotovu, na kikundi cha yule aliyelaniwa, ……basi ajabu ilioje! Vipi wemekuwa (hawa) wafuasi wa saiba (wenye kuabudu nyota) na majusi (wenye kuabudu moto) na washirikina na wenye kuabudu Masanamu, na wafuasi wa jahmiya na wafuasi wa Firauna, wanamjua Mwenyezi Mungu zaidi kuliko Nabii Mussa." HADI AL-RWAH ILA BLAD AL-AFRAH ukurasa wa 210.
Sasa tumulize Ibn Al-qayyim: ikiwa mtu akisema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani naye ana ushaidi wa wazi katika Qur'ani na hadithi sahihi ni kafiri, mfuasi wa Fir’awna, shetani, hana dini, sasa yeye aliyesema kuwa Mwenyezi Mungu ana miguu miwili, mikono miwili, uso, macho mawili anasahau, adhabu ya moto wa akhera kuna siku itakwisha, je ni mfuasi wa nani? Msomaji na ahukumu kwa uadilifu.
Haya ndio matusi ya Ibn Al-qayyim katika Maimamu wakubwa wa kiwahabi. Na Ibn Al-qayyim huyu kaeka mlango kamili katika kitabu chake hicho ukurasa wa 250, ambao anazungumzia kuwa watu wenye kukataa kuonekana kwa Munmgu watakwenda motoni! Na akatoa aya na kuzifasiri anavyotaka mwenyewe, hata mtu aliyesoma tafsiri moja na kitabu kimoja cha nahau anastaajabu na jinsi anavyotoa ushahihdi katika Qur'ani: aya zinasema vyengine na yeye anasema vyengine!!! Kwahivyo kama Imam anatoa matusi kama haya kwa Waislamu leo ukisikia mtu kama Al-tahan au Bim Baz anasema kuwa "mtu anayekataa kuonekana kwa Mwenyezi Mungu ni kafiri" basi usistaajabu; Maimamu wao ndio wana tabia kama hio je wao maamuma watakuwa vipi?
MSIMAMO WA MAIBADHI.
BIN BAZ AKUMBANA
NA AL-KHALILI.
Sh. Ahmad bin Hamed Al-khalili Mufti wa Oman ni mwanachuoni mmoja anayejulikana sana kwa elimu yake na ucha Mwenyezi Mungu wake na tabia nzuri sana za kupigiwa mfano, na jinsi anavyo waheshimu wanavyuoni wa madhehebu nyengine zote na jinsi anvyo wapenda Waislamu na umoja wa Waislamu wote. Na kwa muda mrefu amekuwa akivumilia maneno wanayo yasema hawa Mawahabi juu yake na madhehebu yake, na alikuwa hajihusishi kabisa na kuzungumzia chochote katika tafauti za kimadhehebu, bali katika vitabu vyake na mihadhara yake hunukuu maneno ya Maimamu wa madhehebu zote. Na kila mwenye kufatilia mihadhara yake ataliyona hili. Hata ukisoma katika tafsiri yake "جواهر التفسير" (JAWAHIR AL-TAFSIR) juzuu ya 1 utaona anavyo yanukuu maneno ya Ibn Taymiyya na kuyaheshimu pamoja na kumuheshimu yeye mwenyewe, ingawa hakubaliani naye kabisa katika itikadi. Lakini wenzake ikawa hawakupenda kuichukua fursa hii ya kuheshimiana: ikawa kila muhadhara unaowekwa basi ni kuhusu "Ibadhi na Wanavyuoni wao." Mpaka ilipofika mwezi wa mfunguo sita mwaka wa 1406 A.H. Sh. Al-khalili akapata mualiko kutoka katika wizara ya uadilifu (wizara ya mambo sharia ya kiislamu) ya Saudia. Akatoka yeye na kikundi cha wanavyuoni wa Oman. Walipofika Saudia Mufti wa Saudia Sh. Bin Baz akawaalika katika Ofisi yake. Wakaitikia mwito wakaenda kuonana na Sh. Bin Baz. Sh. Bin Baz akamwita Sheikh Al-khalili pamoja na wenzake ndani, wakaingia watu wawili - Sh. Al-khalili na Naibu wake, Sh. Said bin Khalef Al-kharusi. Sh. Bin Baz akamwambia Sh. Al-khalili "nyinyi Maibadhi, na Mashia, na Al-ashaira (Masuni kama walioko Afrika nzima takriba) na Matridia (Masuni kama waliko India na Pakistan wa madhehebu ya Al-hanafi), basi nyote nyinyi katika itikadi mumepotea." Na Sh. bin Baz akawa katika upande wa Ibadhi anazungumzia zaidi mas'ala hii ya kuonekana kwa Mwenyezi Mungu. Sh. Al-khalili akamwambia kuwa "tafauti hizi hazikuzaliwa leo bali zipo kwa muda mrefu." Ikawa Sh. Bin Baz anaendelea kuwasema Maibadhi kuwa ni wapotovu. Sh. Al-khalili akamjibu kwamba kama uko tayari basi natufanye mjadala wa wazi karibu na msikiti mtakatifu wa Maka, na mjadala huo uwe kwa ajili ya kutafuta haki tu: uwe mbali na kasumba za kimadhehebu, na redio zote na vyombo vyote vya habari virushe moja kwa moja ikiwemo redio Maka na mjadala huo uwe wazi kwa kila anayetaka kushiriki. Sh. Bin Baz akakataa. Sh. Al-khalili akamuuliza "unaonaje kama atakujia mkiristo au myahudi akakwambia mufanye mjadala wa wazi je utakubali? Akasema Sh. Bib Baz "ndio." Akamuuliza Sh. Al-khalili "kwanini basi hutaki sisi tufanye mjadala?" Sh. Bin Baz akasema kuwa "jambo hili linaeneza biadaa." Sh. Al-khalili akamwambia la, jambo hili linaiuwa bidaa na kuiacha dini safi kwa sababu kila mtu atajua ukweli uko wapi." Bin Baz akakataa na kusema kwamba "watu wa bidaa hawakubali kuwachana na bidaa zao." Sh. Al-khalili akamwambia "nimelihakikisha hili kutokana na msimamo wako huu." Na mwisho Sh. Al-khali akamwambia Bin Baz "kama wewe unasema uko kwenye haki na sisi tuko kwenye batili, basi twende pale mbele ya Al-kaaba tukamuombe Mwenyezi Mungu amlani aliyeko kwenye batili." Sh. Bin Baz akakataa. Na Sh. Al-khalili akaondoka hali ya kuwa Sh. Bin Baz kakasirika.
Hapa ukitazama msimamo wa wanavyuoni wa kiibadhi kwa jicho la utafiti na moyo wa kutaka kujua ukweli, basi itakubainikia kuwa ni watu wenye kumiliki hoja za haki na wao wana yakini juu ya itkadi yao kiasi cha kwamba wako tayari kwenda mbele ya Al-kaaba kumuomba Mwenyezi Mungu abainishe haki. Na hivi ndivyo alivyo amrishwa Mtume (S.A.W.) afanye kwa wale waliompinga baada ya kuwa amewasimamishia hoja. Anasema Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitakatifu, akimuamrisha Mtume wake:
فمن حاّجك فيه من بعد ما جائك من العلم فقل تعالوا ندع أبنائنا و أبنائكم و نسائنا و نسائكم و أنفسنا و أنفسكم ثم نبتهل فنجعل لعنة الله على الظالمين"
"Basi wanaotaka kujadiliana na wewe (sasa) baada ya kuwa elimu imekufikia, basi waambie njooni tuwaite watoto wetu na wato wenu na wanawake wa kwetu na wanawake wa kwenu na sisi na nyinyi kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo."
Sura ya 3 aya ya 61.
Kwahivyo Al-khalili akamtaka Bin Baz ambaye kawaita Maibadhi makafiri, wende mbele ya Al-kaba Takatifu wakaombe hivi hivi, lakini Bin Baz akaogopa. Na hii inatosha kuonesha kuwa hata yeye mwenyewe Sh. Bin Baz hana hakika na itikadi yake. Na kama si hivyo kipi kimemzuia kumtaka Mwenyezi Mungu aibainishe haki baina yake na watu ambao kawaita makafiri.
AL-KHALILI ATANGAZA MJADALA.
Kisha baada ya muda si mrefu Sh. Al-khalili akatunga kitabu chake mashuhuri "AL-HAQU AL-DAMIGH" (OVERWHELMING TRUTH) ambacho kinajadili masala matatu ya itikadi kwa kielimu kabisa na kwa hoja za uwazi. Na baada ya kuandika kitabu hiki alipata barua kwa wingi kutoka kwa wasomi mbali mbali kwamba wamekubaliana naye. Na katika kitabu hicho ametoa msimamo wake wa wazi kuwa yuko tayari kujadiliana na mtu yeyote lakini kwa sharti ya kutafuta haki na uwe mjadala wa kujenga umoja wa kiislamu sio mjadala wa ugomvi. Anasema:
"و أعلن للذين لا يرون إلا حسم الخلاف في هذه القضايا حتى تتفق فيها عقيدة الأمة ، بأنني لا أستنكف من الحوار الموضوعي الهادي الهادف ، الذي لا ينشد به إلا الحق ، و لا يفضي إلا إلى تجلي الحقيقة وظهور برهانها، ثم لا يؤدي إلا إلى الألفة والمودة بين المسلمين".
"Na ninawatangazia wale (wote) ambao hawaoni (kitu bora) isipokuwa kuziondoa tofauti katika mas'ala haya ili itikadi ya uma ikubaliane (iwe moja), kwamba mimi sikatai mjadala wa kielimu, wa utulivu na wenye lengo, ambao haitafutwi kwa mjadala huo isipokuwa haki, na wala haupelekei isipokuwa kwenye uwazi wa uhakika na kudhihiri hoja zake, kisha haupelekei isipokuwa kwenye mshikamano na mapenzi baina ya Waislamu."
Al-khalili (AL-HAQU AL-DAMIGH)
ukurasa wa 229.
AL-QANNUBI ATANGAZA
MDAHALO (MJADALA).
Mwanachuoni mwengine mkubwa wa madhehebu ya kiibadhi aliyedhihiri Oman sasa hivi ni Al-imamu Said bin Mabruk Al-qannubi. Huyu ni kijana mdogo sana mwenye umri wa miaka kama 34 tu, lakini ni bahari ya elimu. Utajua elimu yake ukisoma kitabu chake AL-TUFAN AL-JARIF anachomjibu mmoja katika mashekhe wa madhehebu ya kiwahabi ambaye alimsema kwa sababu ya kitabu chake AL-SAIF AL-HAD. Sh. Said huyu anazingatiwa kuwa ni miongoni mwa watu waliofikia daraja ya ijtihadi. Naye amekuwa akijibizana sana na Mawahabi. Na katika maneneo yake kuna tangazo rasmi la mjadala wa wazi baina yake na wao. Anasema Al-imamu Said Al-qannubi katika kitabu chake AL-SAIF AL-HAD ukurasa wa 12:
و نحن نتحدى هؤلاء الحشوية أن يأتوا لنا برواية صحيحة فيها تصريح بالإستقرار أو الإستواء الحسي و ليستظهروا على ذلك بمن يشاء و لو بالثقلين جميعا كما أننا نتحدى أرباب هذه النحلة للمناظرة في هذه المسألة أو غيرها من المسائل الإعتقادية"
"Na sisi tunawachalenj hawa Mahashwiya (Mawahabi) watuletee riwaya sahihi ambayo ndani yake kumesemwa kwa uwazi kuwa (Mwenyezi Mungu) anakaa kitako kweli kweli, na wamuombe msada yeyote wanayetaka hata binaadamu wote na majini wote. Kama vile ambavyo tunawachalenj kufanya mjadala katika mas'ala hii au mas'ala nyengine yoyote ile ya itikadi."
Na anasema katika AL-TUFAN AL-JARIF juzuu ya 3 sehemu ya 1 ukurasa wa 57 akiwatangazia mjadala juu ya itikadi ya kuonekana kwa Mwenyezi Mungu, akasema:
و قد دعوناكم للمناظرة في ذلك أكثر من مرة فأبيتم و هانحن أولاء نكرر لكم ذلك فإن كنتم على استعداد لذلك فهلم إلى المناظرة بشرط أن تنقل بالوسائل الإعلامية , وسيعلم حينها أي الفريقين أحق بالأمن و أهدى سبيلا
"Na tumekuiteni kwenye m jadala zaidi ya mara moja mukakataa, basi na hapa sisi tunakurudieni tena katika hilo: kama muko tayari kwa hilo na twende katika mjadala kwa sharuti kwamba uchukuliwe na vyombo vya habari, basi hapo litajulikana lipi katika makundi mawili linastahiki amani na liloongoka."
Mpaka leo hakuna Sheikh yeyote wa kiwahabi aliyejitokeza: kazi yao ni kukaa peke yao wakiwatukana Waislamu wa madhehebu nyengine, lakini hawako tayari kuutafuta ukweli.
Sasa baada ya haya ndugu Muislam, ningependa ujue kuwa mimi nimekuandikia Mwenyezi Mungu alichonijaalia ili kukufikishia itikadi sahihi aliyoifundisha Mwenyezi Mungu katika Qur'ni na akaifundisha Mtume (S.A.W.) katika hadithi zake sahihi. kwahivyo ninachokuomba ni kuwa ukisome kitabu hiki kwa moyo mkunjufu wa kutaka kujua ukweli tu. Na baada ya kukisoma itakuwa moja katika mawili: ama utakubaliana na mimi kwamba itikadi sahihi ni kuwa Mwenyezi Mungu kama alivyokuwa haonekani duniani vile vile hatoonekana akhera; au utakhitalifiana na mimi katika hili. Ikiwa utakubaliana na mimi, basi jukumu la kuufikisha ujumbe kwa wengine liko katika mikono yetu sote: chukua fursa hii kwa kuwafikishia watu itikadi hii sahihi. Kwa sababu yuko mmoja katika Mashekhe wetu wa Zanzibar ambaye mwanzo alikuwa na itikadi ya kuonekana kwa Mwenyezi Mungu, akapewa kitabu cha Sh. Al-khalili kuhusu mas'ala hii. Akakisoma na baadae akamwambia yule aliyempa hicho kitabu kuwa "kweli Mwenyezi Mungu haonekani lakini usiwambie watu kama mimi nimesema hivi!!!" Jambo hili ni baya sana. Mwenyezi Mungu anasema "na ni nani aliye dhalimu zaidi kuliko yule afichae ushahidi utokao kwa Mwenyezi Mungu." Sura ya 2 aya ya 140. Kwahivyo mimi si mtaji ni nani lakini ikiwa atasoma kitabu hiki basi mwenyewe atajijua. Tunamuomba awache mara moja tabia ya kuficha kitu anachokiitakidi kuwa ndio haki: na kila analolijua kuwa ndio haki basi aliseme.
Na kwa upande mwengine unaweza ukawa hujakubaliana na mimi. Katika hali hii ninakunasihi umuelekee Mwenyezi Mungu kwa sala ya istikhara umuombe akuoneshe au akupe ilhamu juu ya itikadi hizi ipi ni sahihi: wachilia mbali kasumba ya madhehebu na utafute haki bila ya kusita. Yuko mtu ambaye alikaa msikitini mwezi wa Ramadhani kwa muda wa siku nne na huku anasali sala ya istikhara kumuomba Mwenyezi Mungu amuoneshe njia njia ya kufata. Naam, ilipofika siku ya nne akashikwa na usingizi mzito. Na wakati yumo kwenye usingizi kutahamaki anaona nuru kubwa inaingia na mtu mwenye haiba kubwa kava jokho. Akampa mkono, tahamaki ni Mtume (S.A.W.) akambanishia wapi afate. Huyu ni MASUD BIN MUHAMMAD AL-MIQBALI, na habari zake hizi ni maarufu Omani, naye katoa kaseti nzima anaiita " قصة عودتي" (kisa cha marejeo yangu), anaelezea ndani yake habari hizi. Kwahivyo wewe Muelekee Mwenyezi Mungu kwa moyo wa ukweli na wewe utaona haki iko mbele yako. Na hivi ndivyo Mtume (S.A.W.) alivyo wafundisha Masahaba kuwa wamuelekee Mwenyezi Mungu kwa istikhara katika dini yao na dunia yao.
KITABU HIKI.
Katika kukiandika kitabu hiki nimejiongozea sana kwa iktabu AL-HAQ AL-DAMIGH cha Sh. Al-khalili. Kuna sehemu nyengine nimezinukuu moja kwa moja kutoka katika kitabu hicho, na kuna sehemu nyengine nimeziletea maana tu na kuna nyengine nimechukua ushahidi tu na nikauelzea kwa kadiri ya uwezo wangu. Na huo ni katika upande wa aya za Qur’an: si katika utafiti wa hadithi.
Katika sehemu hii ya hadithi utaona humu kuwa hakuna hata hadithi moja katika hadithi hizi walizozitolea hoja wale wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu ataonekana, ilio sahihi: zote zimepokewa kutoka kwa wapokezi waongo, wenye kugushi na madhaifu. Na utaona kuwa riwaya hizi ni nyingi sana na nyengine ni refu sana, nyengine kama karatasi mbili na nusu, na aghlabu ya hadithi za kutunga ziko hivyo. Sasa ukija katika upande mwengine wa wale wenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu haonekani utakuta wana hadithi chache sana ambazo wanazitegemea kwa itikadi yao hio, na zote ni sahihi. Na yote haya yatakubainikia ukisoma kitabu hiki kwa moyo mkunjufu. Soma kitabu hiki kwa moyo mkunjufu: kwa nia ya kutaka kutafuta ukweli.
Na la mwisho ni kuwa katika kusoma kitabu hiki basi usitazame ufundi wa lugha: mimi naadika kiswahili kama lugha yangu tu sina utaalam wa kiswahili hata kidogo, kwahivyo wewe tazama maudhui tu.
Ibn Mohd Al-mazrui.
Tarehe 9/mfunguo 7/ 1422 sawa na 1/7/2001.