SEMINA YA VIONGOZI DINI, VYAMA VYA SIASA, VYOMBO VYA DOLA NA VYOMBO VYA SHERIA.

 

MADA

UMUHIMU WA AMANI NA UTULIVU KATIKA JAMII

 

Imeandaliwa na:

Sheikh Abdulla Talib Abdulla  Kamisheni ya Wakf na Mali ya Amana  Zanzibar.

 

UTANGULIZI:

 

Sifa njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu amabe kwa uwezo wake na nguvu zake tuweweza kukusanyika hapa ili kujadili swala muhimu linaloihusu jamii yetu nalo ni kudumisha amani na utulivu. Sala na salam zimshukie Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na wafuasi wake wote hadi siku ya kiama. Aidha natowa shukrani zangu za dhati kabisa kwa wale wote waliochangia kwa namna moja au nyengine katika kufanikisha mkusanyiko huu. Ninamuomba Mwenyezi Mungu aziweke juhudi zao hizo katika mizani ya mema yao – Amin.

 

Amesema mwanachuoni Ibnu Khaldoun: “Kwa hakika kuwepo jamii ya mwanadamu ni jambo la msingi na la umuhimu mno, kwani binadamu ni mwanajamii katika maumbile yake, anazaliwa katika jamii, anaishi na kufia humo”.

 

Kwa msingi huo, ikiwa jamii ni jambo la lazima kwa mwanadamu ambalo haepukani nalo, nayo ndio inayojenga mustakabali na hadhi ya mwanadamu kuanzia kwake binafsi na mbele ya jamii nyengine basi ni lazima jamii hiyo itunzwe na ienziwe ili idumu katika uasili wake ambao ni mapenzi, amani, utulivu na umoja. Amesema Mwenyezi Mungu: ((Enyi watu mcheni Mola wenu ambae amekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akaumba katika nafsi hiyo mkewe, na akaeneza kwa wawili hao wanaume wengi na wanawake wengi)) {Suratul Nisai aya ya 1} Na akasema tena ((Kwa hakika sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamme mmoja na mwanamke mmoja na tukakujaalieni mataifa na makabila mbali mbali ili mjuane, hakika mbora wenu mbele ya Allah ni yule mchaji zaidi)) {Suratul Alhujurati aya ya 13}.

 

Jamii yetu imejengwa na wafuasi wa itikadi, imani na mitizamo tofauti katika nyanja za dini, siasa, fikra n.k. mambo haya yamo ndani ya nyoyo zetu na ni katika uhuru aliotupa Muumba wa kujichagulia njia tunayopenda kama alivyosema ((Hakuna kulazimishwa katika (kufuata) dini)) {Suratil Baqara aya ya 256}. Pia kunapelekea kujuana kulikotajwa katika aya 13 ya Suratul Hujurat tuliyoitaja  hapo kabla, ya kuwa huyu ni wa dini fulani, madhehebu fulani, chama fulani, mlengo kadha…. Hata hivyo bado sote tutabaki kuwa ni watu wa jamii moja ambao yapo mambo yanayotuunganisha na hatupingani kwayo kwa kutuletea faida kwa sote au hasara na ufisadi kwa sote. Kati ya mambo hayo muhimu ni suala la Amani na utulivu katika jamii yetu.

 

 

MISINGI ILIYOWEKWA NA DINI KATIKA KUDUMISHA AMANI NA UTULIVU

 

Dini ni mfumo na utaratibu wa maisha uliowekwa na Muumba ili kutawala maisha ya mwanadamu. Kwa vile mwanadamu ni mwanajamii kwa maumbile yake ni lazima awekewe mfumo na utaratibu unaoeleweka unaoongoza mwenendo wa jamii hiyo na kulinda maslahi ya wanajamii wote. Kutokuwepo kutokufuatwa au kutokusimamiwa vyema mfumo huu na wanajamii hasa wenye mamlaka ya uongozi kutapelekea kutoweka kwa amani na utulivu katika jamii na badala yake jamii itaishi kama wanayama katika mfumo wa mwenye nguvu mpishe”.

 

Uislamu ukiwa ni katika mifumo ya maisha umeweka utaratibu ambao unachunga maisha ya wanajamii na ulimwengu mzima waishi kwa amani na utulivu ambao umejengwa juu ya msingi wa itikadi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu yaani tawhidi. Msingi unamuainisha kila mwanadamu katika jamii, cheo chake (utukufu wake), lengo la kuumbwa kwake, na mahusiano yake na Muumba na vyote vilivyomo duniani. Itikadi ndio ilani na dira ambayo inatakiwa iongoze fikra na matendo ya mtu aliyejikubalisha kuwa muislamu na kuongoza kila jambo lake la siri na dhahiri.

 

Itikadi ya kiislamu imeweka mambo matano ambayo yanatakiwa kuchugwa sana katika jamii ili kudumisha amani, utulivu na maisha mazuri kwa wanajamii, mambo hayo yanayojulikana kamadharuratul-khamsa” ni:

·        Kuhifadhi dini

·        Kuhifadhi nafsi (maisha ya mwanadamu)

·        Kuhifadhi mali

·        Kuhifadhi heshima za watu

·        Kuhifadhi akili

 

KUHIFADHI DINI:

 

Dini kama tulivyotangulia kuieleza ni mfumo wa maisha. Mfumo huu unakusanya itikadi sheria na tabia. Uislamu umesisitiza itikadi ipandikizwe, sheria zisimamiwe na tabia ziendelezwe ili dini ipate kudumu, kuhifadhika na kuleta maslahi kwa wanajamii.

 

Kwa mnasaba wa mkusanyiko wetu huu, jamii yetu imejiwekea mfumo uliowazi na unaoeleweka ambao unatoa haki, majukumu, na kupanga mahusiano na maingiliano ya wanajamii, mipaka hii ndio inayotakiwa ielekeze tabia na mienendo ya wanajamii wote.

 

Kila mmoja kati yetu anahusika kwa namna fulani katika uanzishwaji, usimamizi na utekelezaji wa mfumo huu. Na mafunzo ya dini yanatufunza kuwa ataulizwa na Mwenyezi Mungu ni kwa namna gani ameisimamia dhamana yake kama ilivyokuja katika hadithi “Nyote ni wachunga na kila mmoja ataulizwa kuhusu kile alichokichunga”. Hivyo ili kudumisha amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kinachotukabili kila mmoja ni lazima atekeleze wajibu wake ipasavyo kwa kuzingatia sheria na miongozo iliopo kwani kama tunavyoelewa kuwa wanajamii huathiriwa na uzuri au ubaya wa mfumo wa jamii kama wanavyoathiriwa na sera na matendo ya viongozi wao.

 

Tukiwa ni viongozi tuliopewa hatamu na tuangalie vyema wapi tunaipeleka jamii yetu na kwa faida ya nani? Tujiepushe na kufuata matamanio ya nafsi zetu ili tufuate sheria na taratibu zilizopo huku tukizingatia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema: ((Na lau kama haki (sheria) ingefuata matamanio yao basi vingeharibika (vilivyomo) mbinguni na ardhini)) {Al-Muuminun aya ya 71}.

 

KUHIFADHI NAFSI:

 

Nafsi ya mwanadamu imetukuzwa sana na muumba kama alivyosema ((Bila shaka tumemkirimu mwanadamu)) {Suratul Israa aya ya 70}. Aidha kuiua nafsi au kufanya chochote kitakachopelekea kufisidika kwa nafsi hata kama bado imo tumboni linahesabika kuwa ni kosa na dhambi kubwa sana. Amesema Mtukufu (Atakaeiua nafsi bila ya nafsi au kufanya ufisadi katika ardhi (atakaopelekea kuungamia kwa nafsi) basi ni sawa na aliewaua watu wote)), {Al-An-am aya ya 73}.

 

Ikiwa hali ndio kama hii tuelewe kuwa kuua sio kwa kupiga bunduki au mshale tu, lakini ishara tu au neno moja, linaweza kuwa ndio sababu ya ufisadi mkubwa na kuhiliki kwa maisha ya wanadamu wengi. Aidha mtu hatoweza kujivua mbele ya Mungu kwa kosa ambalo yeye ndie sababu au ana mchango fulani wa kutokea kwake. Maandiko yanasema kuwa mtoto wa Adamu bado hupata fungu lake la dhambi kwa kila nafsi inayouliwa kwa vile yeye ndie asili ya tendo hilo. Jee sisi tumejiandaa vipi kuiepusha jamii yetu ili isije ikatumbukia katika madhambi haya makubwa kutokana na kauli zetu au matendo yetu?.

 

Tutambue kuwa sote ni watu wa jamii moja na asili ya wanaadamu wote ni moja kama tulivyokwishaeleza. Kutofautiana kwetu kwa nasaba koo, makabila, rangi, majimbo, visiwa vyetu, itikadi, vyama, mitizamo, vyeo n.k. ni sawa na lilivyogawanyika mti na matawi yake lakini shina ni moja. Vile vile kila mmoja ana umuhimu na mchango katika kuendeleza jamii yetu hata kama dhahiri tutaona kuwa tunapingana.

 

Mwenyezi Mungu kwa kumtukuza mwanadamu amempa akili na kipaji ili aweze kujiletea maslahi katika dunia yake na akhera yake. Hivyo akili yake inapomuongoza katika itikadi, fikra, mtizamo tofauti na ulizonazo wewe tunatakiwa kuvumiliana au kushindana kihoja na kujiepusha na kila litakaloleta madhara kama alivyosema Mtume S. A. W ((Hakuna madhara wala kudhuriana)).

 

Mwenyezi Mungu amrehemu Sayyidna Omar aliposema lau kama mbuzi aliyeko Iraq atampiga pembe mbuzi mwenzake basi ninaogopa asije akaulizwa Omar (ilhali yeye yuko Madina)” tuyazingatieni vyema maneno haya na kuzihesabu nafsi zetu kabla hatujahesabiwa.

 

 

 

 

KUHIFADHI MALI:

 

Mali ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya jamii yoyote. Mwenyezi Mungu ameitaja aliposema ((Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Allah amezijaalia kwa ajili ya maisha yenu)) {Nisai aya ya 5}. Aidha mali ikiwa ni katika mapambo ya maisha ya dunia ((mali na watoto ni mapambo ya maisha ya dunia)) zina fitna kubwa na ni miongoni mwa sababu kubwa zinazopelekea kuvunjika kwa amani katika jamii na nchi nyingi.

 

Ikiwa kuhifadhi amani na utulivu katika jamii yetu suala la mgawanyo wa rasilimali za taifa ni lazima lizingatiwe sana. Vile vile njia za kupata vipato vya halali zizidishwe na zile zote zinazoleta dhulma kama rushwa, riba, wizi, unyang’anyi n.k. ni lazima zipigwe vita kwa nguvu zote.

 

Mali ikiwa ni kidogo au nyingi ina thamani kubwa kwa mwenyewe na kuharibiwa kwake kuna athari mbaya sana, motokeo ya kuchomwa moto nyumba, kuharibiwa mazao au mali za watu binafsi na serikali limekuwa ni jambo la kawaida katika kipindi kama hiki, lakini ukitafakari ni kwa faida ya nani? Jamii inapokuwa na watu wenye nguvu kiuchumi n.k. ndiyo nayo inavyokuwa na nguvu kiuchumi, kijamii na kuweza kuziathiri jamii nyengine. Vinginevyo itazidi kuwa dhaifu na kuathiriwa na jamii nyenginezo zenye nguvu katika kila nyanja.

 

Tukiwa ni viongozi na wenye dhamana muhimu katika taasisi zetu tujitahidi kulinda mali zetu pia za watu na taasisi nyengine ili kudumisha amani na utulivu uliopo. Mtume anatuasa kuwa “hautoondoka mguu wa mja siku ya kiama mpaka aulizwe kuhusiana na mambo manne …. na mali yake wapi ameichuma na vipi ameitumia ….”

 

Hivyo katika kuhifadhi mali kunaingia pia katika suala zima la matumizi. Watu wasifanye ubadhirifu au baadhi ya kusahauliwa mfano masikini na miradi mbali mbali ya maendeleo. Aidha amali zetu zifungamane na ihlasi ili matendo yetu yatupe faida duniani na akhera na yawe mbali na ria au maslahi ya kidunia tu.

 

KUHIFADHI HESHIMA ZA WATU:

 

Dini inatutaka kuheshimiana na kutodharauliana kwa itikadi, uwezo fikra, mitizamo n.k. Tunatakiwa tuwaheshimu watu kwa vile ni binadamu alietukuzwa mbele ya Mwenyezi Mungu, na ana haki na uhuru wa kufuata mtizamo mwengine au kufanya tendo lolote madhali hatokiuka sheria na taratibu zilizopo.

 

Kwa msingi huu dini imeweka kipimo cha uadilifu kuwa ndio kinachonyanyua shakhsia ya mtu au kikundi na sio ukoo, kabila, jimbo, jinsi, chama au itikadi. Aidha dini imesisitiza tabia njema na kukataza yote yanayovunja heshima za watu, ikiwemo kudhalilishwa, kusingiziwa uongo, kusengenywa, kutukanwa n.k. Amesema Mtume S. A. W: ((Kumtukana muumini ni ufasiki na kumpiga ni ukafiri)). Kama ambayo Mwenyezi Mungu aliwakataza waislamu kuwatukana Miungu ya washirikina ili jambo hilo lisije likapelekea kuvunjika kwa amani na utulivu na kukaenea tabia ya kutukaniana Miungu (Wala msiwatukane wale ambao wanawaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu wasije wakamtukana Allah kwa jeuri (uadui) na bila ya elimu)). {Suratul Al-Anam aya ya 111}.

 

Katiba za nchi yetu na miongozo ya vyama na taasisi zetu zinaamini na kuahidi kutetea haki za binaadamu hivyo kila mmoja wetu na atekeleze wajibu wake ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu unadumishwa kwa maslahi ya jamii nzima. Tulinganie sera zetu kwa kadiri ya uwezo wetu na tuwe tayari kusahihishana na kurekebishana kwani hakuna mkamilifu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo kusahihishana, kukosoana na kuelekezana ni lazima kuwe kwa heshima na meneno mazuri na sio vyenginevyo kwani sote tuko kwenye jahazi moja na likitoboka tutaghariki sote.

 

KUHIFADHI AKILI:

 

Akili ni nyenzo ambayo inamtofautisha mwanadamu na mnyama kwa vile ndio inayomuwezesha kufikiri. Akili inatakiwa kuhifadhiwa kwa kukuzwa kielimu na kimaarifa. Vile vile kukingwa na yote yatakayoweza kuifisidi na ndio maana ukaharamishwa ulevi wa namna zote na mafunzo yote mabaya.

 

Mwenyezi Mungu ametupa dhamana katika jamii yetu, wanajamii wanatufuata na kutusikiliza hivyo ni lazima tuwe makini katika yale tunayoyapandikiza kwa wafuasi tusije tukapotea au kupoteza. Amesema Mtukufu ((Jee ndio yanayotarajiwa kwenu wakati mkipata ukubwa kufisidi katika ardhi na kuwakata jamaa)) Muhammad aya ya 22. Tutambue kuwa sera na matendo yetu yatakapokwenda kinyume na maamrisho ya dini Mwenyezi Mungu hatotuacha kama alivyosema ((Na wanayakata yale ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha yahifadhiwe na wanafanya ufisadi katika ardhi hao watapata laana na watapata marejeo mabaya)) Raad aya ya 25.

 

HITIMISHO

 

Migogoro ni sababu kubwa ya kudumaa na kuvia maendeleo ya jamii yoyote. Jamii inapokosa amani na utulivu migogoro na fujo ndio hushika hatamu na jamii huporomoka katika kila nyanja na kudharaulika mbele ya jamii nyengine. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu ((Wala msizozane (msigombane) msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu zenu, na vumilieni (mstahamiliane) bila shaka Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaovumilia)) {Al-Anfal aya ya 46).

 

Katika karne tuliyonayo ya sayansi na teknolojia ulimwengu umekuwa kama kijiji kimoja. Hali hii imepelekea kinyang’anyiro kikubwa baina ya jamii, nchi na jumuia katika kila nyanja. Kila jamii inatetea matakwa na maslahi yake yapate kufanywa aula ili kujihakikishia kuwa kinapata nguvu, uhai, maendeleo ya kiuchumi, maendeleo ya kisiasa, ustawi wa jamii, ushirikishwaji na kujipanua.

 

Dunia imeshuhudia walimwengu wakikimbiana katika nguvu za kielimu, kisiasa, kiuchumi na kuitamaduni. Wazanzibari na Watanzania hatukusalimika katika kinyang’angiro hicho nasi tuna nafasi kubwa ya kuipeleka mbele jamii yetu au huisababisha kubanwa kipembeni na kutoweza kupumua vyema.

 

Ni lazima tufikiri mara nyingi kabla ya kusema au kutenda tuweke mbele maslahi ya nchi na watu wetu, tujuwe kuwa matendo yetu yatasajiliwa na historia na kizazi kijacho kitatuhukumu kwayo ima vyema au vibaya. Na mwisho wa maisha yetu mafupi ni kuingia kaburini kuanza maisha ya milele. Mauti yatatuenea sote, kaburi litatubana sote na kwa Mwenyezi Mungu tutarejeshwa sote akatuhukumu kwa haki nae ni mbora wa mahakimu.

 

Tunamuomba Allah atupe amani na utulivu katika nchi yetu.